Visit Sponsor

Written by 8:47 am KITAIFA Views: 47

WATOTO 45 KUFANYIWA UPASUAJI MOYO

Watoto 45 wenye magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo yakiwemo
matundu kwenye moyo, na matatizo ya mishipa ya damu kufanyiwa upasuaji wa
moyo katika kambi maalum inayofanywa na wataalamu wa afya wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la
Mending Kids lililopo nchini Marekani.
Kambi hiyo maalumu ya siku tano ilianza jana na kutoa matibabu ya upasuaji wa
moyo wa tundu dogo kwa kutumia mtambo wa cathlab kwa watoto 25 na
upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua kwa watoto 20.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo
kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Stella Mongela alisema
upande wa cathlab watoto 25 watapatiwa matibabu ya kuziba matundu
mbalimbali yaliyopo katika kuta za moyo pamoja na kufungua mishipa ya damu
iliyobana inayopeleka damu kwenye mapafu na kwenye mwili.
Dkt. Stella alisema kupitia kambi mbalimbali zinazofanyika JKCI zimekuwa zikitoa
fursa kwa madaktari wazawa kuendeleza ujuzi wao kwani wamekuwa wakikutana
na mabingwa waliofanya kazi kwa muda mrefu hivyo kuongeza ujuzi zaidi.
“Kambi ya wataalamu wa afya kutoka Shirika la Mending Kids ni moja ya kambi
inayotupa nafasa wataalamu wa JKCI kujifunza mbinu mbalimbali za kutoa
huduma bora za matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto”, alisema Dkt. Stella
Kwa upande wake Daktari bingwa wa upasuaji mkubwa wa moyo kwa watoto
kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Felix Shonyela alisema Idara ya
upasaji mkubwa wa moyo imepanga kuwafanyia upasuaji wa moyo watoto kati ya
watatu hadi wanne kila siku wakati wa kambi hiyo maalumu.
Dkt. Shonyela alisema wakati wa kambi maalumu watafanya upasuaji wa moyo
kwa watoto wenye magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo yakiwemo matundu
katika moyo na mishipa ya damu ambayo haiko sawa inayopeleka damu kwenye
mapafu.
“Katika kambi hii tutaenda kurekebisha mishipa ya damu ambayo haiko sawa
inayoelekea kwenye mapafu na kupelekea mishipa mingine inayochukua damu

kutoka kwenye moyo kwenda kwenye mapafu kuwa midogo, tunarekebisha
mishipa hiyo ili damu iweze kwenda vizuri kwenye mapafu”, alisema Dkt.
Shonyela
Dkt. Shonyela alisema watoto ambao mishipa yao ya damu haiko sawa mara
nyingi wakiwa wanafanya michezo huchoka kwasababu hakuna mbadilishano
mzuri wa hewa ya oksijeni katika mapafu kwasababu damu inayokwenda katika
mapafu inakuwa kidogo.
Naye mzazi ambaye mtoto wake amefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo katika
kambi hiyo kutoka Mkoani Tanga Herieth Mbelwa alisema wazazi wengi
wamekuwa wakiogopa kusikia watoto wao wanaumwa magonjwa makubwa kama
ilivyo magonjwa ya moyo hivyo kuacha kuwapeleka Hospitali na kuwatibu kwa
miti shamba.
Herieth alisema mtoto wake ana miaka minne na amekuwa akitibiwa shida ya
nimomia hadi mwaka huu alipoamua kufika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete na
mtoto kugundulika kuwa na tundu kwenye moyo.
“Naamini kupitia kambi hii baada ya upasuaji ambao mtoto wangu kafanyiwa jana
utaenda kuondoa changamoto alizokuwa akipitia kama za ukuaji, kutokuongezeka
uzito, kuchoka na kushindwa kucheza”, alisema Herieth
Kambi hiyo iliyoanza jana tayari imeshatoa huduma za matibabu ya moyo kwa
watoto saba ambapo watoto watatu wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo na
watoto wanne wamefanyiwa upasuaji wa tundu dogo kwa kutumia mtambo wa
cathlab.

About The Author

(Visited 47 times, 1 visits today)

Last modified: October 10, 2023

Close