Osaka Kansai-Japan
16 Mei, 2025.
Tanzania imekuwa kivutio na kupongezwa kwa jitihada kubwa ya Serikali na sekta binafsi kuendeleza maeneo ya miundombinu ya ujenzi, mawasiliano na uchukuzi pamoja na miundombinu ya umeme katika maonesho ya Makubwa ya Dunia ya EXPO OSAKA 2025 yanayoendelea katika jiji la Osaka Kansai Japan.
Hayo yameelezwa na Balozi wa Tanzania nchini Japan Mhe .Baraka Luvanda alipofungua rasmi wiki ya miundombinu iliyoanza leo kwa kukaribisha ushiriki wa Taasisi mbalimbali kutoa maelezo kwa wageni wanaotembelea maonesho hayo ikiwa ni mfululizo wa Programu za kila wiki ambazo zimeandaliwa na TanTrade ili kutangaza fursa katika sekta mbalimbali za kiuchumi zinazosimamiwa na Wizara za Kisekta kwa kushirikiana na Taasisi zilizopo chini ya Wizara pamoja na Sekta binafsi kwa uratibu wa TANTRADE kwa kushirikisha Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda-Zanzibar.
Ujumbe wa Tanzania katika wiki ya miundombinu umehusisha ushiriki wa Taasisi mbalimbali ikiwemo TANESCO, Wakala wa Majengo -TBA, TANROADS, TGDC na wengineo.
Mhe. Balozi amesema
“…Nimefungua wiki hii ya pili ili kutangaza na kuonesha mambo makubwa ambayo Tanzania imefanya katika sekta ya miundombinu ya barabara, ujenzi, mawasiliano na uchukuzi pamoja na miundombinu ya umeme ili kuitangaza nchi kwa kuvuta wawekezaji zaidi lakini pia kujipanga katika kuzitambua fursa za masoko na Biashara na hivyo kuimarisha uchumi wa nchi. Ni matarajio yetu tutafanikiwa kupata wadau wa miradi mbalimbali ya kimkakati sambamba na fursa za uwekezaji kwenye miradi mbalimbali yenye tija kwa taifa letu…”
Maonesho hayo ya Dunia yanashirikisha nchi zaidi ya 160 zinazotarajiwa kupata watembeleaji takriban Milioni 28.2 ambao wanatoka Japan na nchi za mataifa mengine Duniani.
Sambamba na Programu ya Wiki za miundombinu kutakuwa na maadhimisho ya Siku Maalum ya Kitaifa kwa Tanzania ambayo itafanyika tarehe 25 Mei , 2025 ikifuatiwa na Kongamano la Biashara, Uwekezaji na Utalii tarehe 26 Mei, 2025 ambapo Nchi itatumia siku hiyo kutangaza fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji, vivutio vya utalii pamoja na mila na utamaduni wa Kitanzania. Mgeni rasmi katika maonesho ya Expo 2025 Osaka anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kasim Majaliwa Majaliwa.
About The Author
Last modified: May 17, 2025