▪️Lengo ni kuwaongezea Watanzania wigo wa uwekaji akiba na uwekezaji kupitia dhahabu
▪️Waziri Mavunde azitaka Taasisi za Fedha kuwawezesha watanzania kimtaji
▪️Afungua Tawi jipya la STANBIC GEITA
▪️Wachimbaji wadogo kukopa fedha isiyozidi 115,000,000 bila dhamana
▪️STANBIC kuja na riba ndogo ya mikopo kwa wachimbaji nchini
*Geita*
Ikiwa ni hatua ya kuwaongezea watanzania wigo wa uwekaji akiba na uwekezaji kupitia ununuzi wa dhahabu, Serikali ipo mbioni kuanzisha uuzaji wa Sarafu ya dhahabu nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 17 Mei, 2025 na Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde (Mb) akiwa Mkoani Geita aliposhiriki katika uzinduzi wa tawi la benki ya Stanbic Geita.
“Mheshimiwa Rais wetu mpendwa *Dkt. Samia S. Hassan* amefanya makubwa katika sekta yetu ya madini, na ndiyo maana tumeweza kuchangia katika pato la Taifa kufikia asilimia 10.1 kwa mwaka 2024, mwaka mmoja kabla ya mwaka 2025 kama ilivyokuwa imeelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi na Mpango wa Maendeleo wa miaka 5.
Wizara kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzanania(BOT) tunajadiliana namna bora ya uanzishwaji wa Sarafu za dhahabu(𝙜𝙤𝙡𝙙 𝙘𝙤𝙞𝙣𝙨) ili kuongeza umiliki wa dhahabu miongoni mwa wananchi, kuimarisha soko la ndani la dhahabu na mzunguko wa fedha ndani ya nchi yetu.
Hatua hiyo ya uanzishwaji wa uuzaji wa Sarafu ya dhahabu ni sehemu ya maboresho ya mpango wa ununuzi wa dhahabu kupitia Benki Kuu ya Tanzania ili kufikia malengo tarajiwa ya kuwa na ununuzi wa dhahabu endelevu na wenye tija nchini.
Nawapongeza Benki ya STANBIC kwa kusogeza huduma rafiki ya kibenki kwa wananchi wa Geita hususani wadau wa madini na hivyo kuzitaka Benki nyingine kuiangalia sekta ya madini kwa upekee ili kuwezesha mitaji kwa watanzania ili washiriki katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini, kwani sekta hiyo ina utofauti mkubwa na sekta nyingine za uzalishaji nchini” Alisema Mavunde
Awali, akitoa maelezo kuhusu uanzishwaji wa Tawi hilo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Stanbic, *Bw. Fredrick Maxi* aliishukuru Serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara na kubainisha kuwa Benki ya Stanbic kwa sasa ina matawi 15 nchini na inaendelea kufungua matawi mengine mengi kwenye maeneo ya uchimbaji ili kuwafikia wadau wengi zaidi kwenye sekta ya madini,na pia Benki inakuja na mpango maalum wa kutoa riba ndogo isiyo ya kibiashara kwa sekta ya madini ili kuchochea shughuli za madini nchini ambapo kwa sasa wachimbaji wadogo wanaweza kuchukua mikopo isiyozidi Tsh 115,000,000 bila kuwa na dhamana.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mh. Martin Shigela aliishukuru benki ya Stanbic kwa kuleta Tawi Mkoani Geita na kusisitiza kwamba, ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwezesha sekta za uzalishaji zinazochochea ukuaji wa biashara na kuzifanya benki za biashara kuchangamkia fursa zinazoendelea kuibuka mkoani hapo na kuwataka wananchi wa Geita kuchangamkia huduma zitolewazo na taasisi hizo za fedha katika kujiimarisha kimtaji.
About The Author
Last modified: May 17, 2025