Na Mwandishi Wetu MWANAHABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewaaga rasmi Mahujaji wa Zanzibar wanaotarajiwa kuelekea katika miji mitakatifu ya Makka na Madina mwaka huu kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Hija huku akiwaasa kushikamana na mafunzo ya dini na kuiombea nchi amani, mshikamano na maendeleo zaidi.
Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo katika hafla maalum ya kuwaaga Mahujaji hao iliyofanyika katika Msikiti wa Jamii Zinjibar, Mazizini, Mkoa wa Mjini Magharibi, leo tarehe 17 Mei 2025.
Ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana kwa karibu na Umoja wa Taasisi za Hija Zanzibar (UTAHIZA) pamoja na Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana ili kuondoa changamoto zinazowakabili Mahujaji na kuhakikisha utekelezaji mzuri wa ibada hiyo tukufu.
Vilevile, Alhaj Dkt. Mwinyi amethibitisha kupokea risala ya UTAHIZA kuhusu changamoto kadhaa, ikiwemo ucheleweshaji wa michango ya Mahujaji, haja ya eneo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya UTAHIZA, na pendekezo la kuanzisha Mifuko Maalum ya Hija. Ameahidi kuwa Serikali italifanyia kazi suala hilo.
Katika hatua nyingine, Alhaj Dkt. Mwinyi ametoa shukrani maalum kwa Shirika la Ndege la Saudi Arabia kwa kuridhia ombi la kuwa na safari za moja kwa moja kwa Mahujaji wa Zanzibar, sambamba na pongezi kwa Ubalozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia kwa mchango wao katika kufanikisha utaratibu huo.
Halikadhalika Alhaj Dkt. Mwinyi amewataka Waislamu wote kuwaombea Mahujaji na kuiombea nchi amani, umoja na maendeleo, akibainisha kuwa mafanikio ya taifa letu yanahitaji mshikamano wa kila mmoja.
About The Author
Last modified: May 17, 2025