Na Mwandishi Wetu MWANAHABARI
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Afrika Kusini Mheshimiwa Thabo Mbeki ameshiriki mjadala wa kuendeleza uchumi wa buluu na utalii Afrika uliofanyika jijini Dar es Salaam na kuendeshwa na kauli mbiu ya “Kuinua Uchumi wa Bluu na Utalii kwa Ajili ya bara la Afrika”.
Majadiliano hayo yalilenga kusisitiza umuhimu wa usimamizi endelevu wa bahari, maziwa, na mito pamoja na kukuza utalii wa kikanda na kimataifa kama nyenzo za kuimarisha uchumi, ajira, na utambulisho wa Kiafrika.
Akizungumza katika mjadala huo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Shaib Mussa amesema Afrika iko katika kipindi nyeti ambacho kinahitaji vitendo thabiti, dhamira isiyotetereka, na suluhisho bunifu na zinapaswa kuelekeza nguvu katika maeneo muhimu. “Hatua si chaguo tena, bali ni lazima zichukuliwe ili kudhibiti maendeleo holela ya maeneo ya pwani.” alisema.
“Ninaamini kuwa majadiliano haya yatachangia katika kuendeleza malengo ya kimkakati ya Afrika ya kuunda, kushirikiana, na kusambaza maarifa. Ninafahamu kuwa tuna timu za utafiti kutoka vyuo vikuu na taasisi mbalimbali za tafiti barani Afrika zinazoshughulika na masuala yanayohusiana na bahari na mazingira ya majini. Katika mkutano huu, watawasilisha mafanikio yaliyopatikana kupitia ushirikiano wao na wenzao kutoka sehemu mbalimbali za Afrika,” alisema.
Aliwasihi washiriki wakumbuke umuhimu wa ushirikiano na kwamba hakuna taifa moja linaloweza kukabiliana na changamoto peke yake na kuongeza kuwa dhamira ya pamoja ya kushirikiana, tukitumia maarifa na uzoefu wetu wa pamoja, ndiyo itakayokuwa msingi wa mafanikio ya mkakati huu na kusisistiza umoja, ubunifu, na kutambua kwamba Waafrika wote ni walezi wa rasilimali muhimu za majini kwa uhai wa viumbe vyote.
Mhe. Thabo Mbeki yuko nchini kwa ajili ya kushiriki programu mbalimbali zilizoandaliwa na Taasisi yake kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya Afrika itakayofanyika tarehe 25 Mei 2025 ambapo Mhadhara wa 15 wa Mbeki Foundation utafanyika nchini tarehe 24 Mei 2025 jijini Dar es Salaam na utawakutanisha wana majumui mbalimbali kutoka barani Afrika .
About The Author
Last modified: May 21, 2025