
Baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuzindua sera ya mambo ya nje ya mwaka 2001 toleo la 2024, Mtaalamu wa masuala ya siasa Dr. Bravious Kahyoza amesema kuwa maboresho yaliyofanyika katika sera hiyo yamekuja kwa muda muafaka.
“Sera hii imekuja wakati muafaka. Kilikuwepo kilio cha muda mrefu kuwa sera yetu ihuishwe kwendana na hali halisi ya dunia. Na hiki ndicho kilichofanyika.” Alisema Dr. Kahyoza.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa sera ya Mambo ya nje ya Tanzania sasa itakuwa na misingi 8 tofauti na misingi 7 iliyokuwa nayo kuanzia mwaka 2021. Rais Samia alizitaja misingi hiyo kabla ya kuongezwa kwa msingi wa nane.
“Moja ni Kudumisha uhuru, dola na kulinda mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mbili ni kudumisha uhuru wa watu, haki za binadamu, usawa na demokrasia, tatu ni kudumisha ujirani mwema, nne ni kudumisha umoja wa afrika, tano ni kudumisha uhusiano ya kiuchumi na wadau wa maendeleo sita ni kudumisha sera ya kutofungamana na upande wowote na ushirikiano na nchi za kusini (South South Cooperation) na saba ni kuunga mkono juhudi za Umoja wa mataifa katika kutatua changamoto za dunia, usalama na amani.” Rais Samia akitaja misingi 7 ya sera.
Rais Samia aliendelea kufafanua kuwa kutokana na mabadiliko ya utandawazi kote duniani, sera hiyo imeboreshwa mwaka 2024na kuongezwa msingi wa nane ambao unalenga kulinda utamaduni wa mtanzania.
“Baada ya maboresho kufanyika mwaka 2024, tumeongeza msingi mmoja ambao ni kulinda na kuendeleza maadili, mila na utamaduni wa mtanzania ikiwemo kukuza na kuendeleza matumizi ya lugha yetu adhimu ya Kiswahili.”
Akizungumzia kuhusiana na sera ya mambo ya nje kote duniani, Dr. Kahyoza amesema kuwa mara nyingi nchi inafanya mabadiliko katika mikakati ya sera ya nje na siyo mabadiliko kwa sababu sera ni misimamo ya taifa husika kuhusu namna inavyotazama dunia.
“Kwa kawaida nchi haibadilishi sera yake ya mambo ya nje. Huwa inabadilisha mkakati wake wa sera ya mambo ya nje. Hii ni kwa sababu, sera ya mambo ya nje ni mwendelezo wa masuala ya ndani ambayo ni misingi ya nchi husika na jinsi inavyoamua kuitazama dunia. Ni tunu zinazoifanya nchi hiyo kuwa na misimamo ya aina fulani miongoni mwa mataifa.”
Katika maboresho ya sera iliyozinduliwa miongoni mwa masuala muhimu ni pamoja na kuongezwa suala la watanzania waishio nje ya nchi(Diaspora), kuongeza suala la Uchumi wa Bluu, kupanga kuitumia Kiswahili kama bidhaa, kuongeza masuala ya mazingira pamoja na mabadiliko ya tabia ya nchi pamoja na masuala ya jinsia na vijana.
Tanzania ina eneo kubwa la uchumi wa Bluu katika bahari ya Hindi ambao unaweza kutoa fursa mbalimbali kwa vijana. Katika kuangazia suala hili na jinsi gani mabadiliko haya ya sera yanaweza kubadilisha maisha ya vijana, Mtaalamu na Mchambuzi wa Uchumi Dr. Kahyoza anasema hii ni hatua muhimu kwa sababu mabadiliko ya sera yatachochea ongezeko la uwekezaji katika sekta za baharini ikiwemo shughuli za uvuvi.
“Mabadiliko haya ya sera yatachochea uwekezaji mkubwa kwenye uvuvi kwenye kina kirefu, kuongeza utalli wa bahari na kuimarisha usafiri wa baharini.Uchumi wa Buluu ni muhimu sana kwa sera ya mambo ya nje kwa nchi yenye rasilimali za bahari kama Tanzania. Kwa hiyo ni uamuzi muafaka. “ Alifafanua Dr. Kahyoza
Kwa upande mwingine. Dr. Kahyoza anasema mabadiliko haya yanaweza kuleta mabadiliko katika mchango wa Uchumi wa Bluu kwa taifa ikiwemo kutoa nafasi zaidi za ajira
“Ni muhimu kwa sababu uchumi wa buluu una nafasi ya kuchangia usd 15 kwa mwaka kwenye uchumi wetu kutoka kiwango cha sasa cha USD 8 ikiwa tutawekeza vizuri. Na unaweza kuajiri zaidi ya watu 360,000 kwenye mwambao wa Pwani kutoka 180,000 wanaofanya kazi kwenye uchumi huo hasa kwenye uvuvi.”
Katika uzinduzi wa sera ya mambo ya nje ya Tanzania Masuala ya mazingira na tabia ya nchi katika uhusiano wa kimataifa yameongezwa katika sera. Katika kufanyia tahmini ya ni kwa vipi suala hili ni muhimu hasa kwa uchumi wa Taifa, Dr. Kahyoza anasema suala la mazingira ni suala muhimu hasa katika dhana ya kutengeneza uchumi endelevu
“Ni muhimu sana kwa uchumi wa kileo. Leo kuna kitu kwenye uchumi kinaitwa New Climate Economy (NCE). Ni uchumi unaotazama hali ya kulinda mazingira ili kuwa uchumi endelevu. Kwa Tanzania hii ni muhimu kwani tafiti zinaonesha, kwa sasa Tanzania inapoteza karibu USD 500 million kwa mwaka kwa sababu ya mabadiliko ya tabia nchi. Hii ni sawa na kati ya 1% mpaka 1.5% ya Pato Ghafi la Taifa(GDP).” Dr.Kahyoza akifafanua kuhusiana na mambo ya mazingira
Miongoni mwa mijadala katika mikutano ya kimataifa kwa sasa ni suala la mabadiliko ya tabia ya nchi. Suala hili linaonekana kuwa haliwezi kupata suluhisho la nchi moja moja na badala yake juhudi za pamoja zinahitajika. Katika hili Dr. Kahyoza ana mtazamo huu
“Kwa hiyo ni suala la maana sasa kuwa na mtazamo wa kukabilana na suala hili hasa kupitia sera ya mambo ya nje kwani changamoto za nje ni kubwa kuliko za ndani. Tafiti hizo zinaonesha kuwa, tusipodhibiti hali hii, mabadiliko ya tabja nchi yanaweza kugharimu uchumi wetu zaidi ya 17% kufika mwaka 2050.”
Wakati wa uzinduzi, ilielezwa kuwa kumefanyika maboresho ya mfumo wa wa wizara ya mambo ya nje ambapo sasa miradi ya kimkakati itaonekana pamoja na masuala ya usajili wa Diaspora yatafanyika katika mfumo huo. Imeelezwa kuwa sasa serikali itaweza kujua idadi halisi ya Watanzania waishio nje ya nchi yaani Diaspora. Tulitaka kufahamu kutoka kwa mtaalamu wa uchumi, Je hatua hii ni muhimu kiasi gani kwa taifa?
“Kuna faida gani kwa uchumi wa Taifa Kujua idadi kunakusaidia kufahamu ni jinsi gani utatumia hiyo rasimali watu iliyo nje ya mipaka ya nchi yako. Inaipa nchi nafasi ya kujaua watu wake wako wapi na wana ujuzi gani ili kuamua iwatumieje au waisaidieje nchi yao.” Maoni ya Dr. Kahyoza kuhusu watanzania waishio nje.
Kutokana na sera mbalimbali kutotekelezwa kwa kiwango kikubwa, sera ya mambo ya nje inategemea juhudi za wataalam kuwaelimisha watekelezaji pamoja na wadau muhimu. Katika hotuba yake Rais Samia aliagiza Wizara ya Mambo ya Nje kuhakikisha inatoa elimu ili kuongeza uelewa juu ya maboresho yaliyofanyika.
Katika eneo la utekelezaji wa sera Dr. Kahyoza alikuwa na mtazamo huu
“Utekelezaji utategemea sana uelewa wa sera yenyewe. Ndio maana Rais ameomba wizara kufanya mafunzo. Lakini pia kuiguisha kwenye mambo ya msingi ya ndani, kama uchumi, michezo na sera za umma kama elimu ili kuwa mifumo ya kijamii iliyo shindani. Hii ndiyo sababu sera hii inasisitiza juu ya Diplomsia ya Umma(Public Diplomacy)”
Maagizo ya Rais
Akizindua sera hii, Rais Samia alitoa baadhi ya maelekezo ikiwa ni pamoja na wito kwa watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora) kuja kuwekeza hapa nchini katika sekta mbalimbali huku akiwaasa kutangaza sifa nzuri za Tanzania.
“Kwa watanzania wanaoishi nje, pamoja na raia wa nchi nyingine ambao wana asili ya Tanzania, kwa kuwa serikali imewatambua kama wabia muhimu wa maendeleo, karibuni nyumbani kwa uwekezaji wa sekta za kiuchumi na kijamii na ni wajibu wenu kuzitangaza sifa njema za Tanzania katika maeneo yenu mnayoishi badala ya kuisema vibaya nchi yenu mlikotoka.”
Kufuatia wito huu wa Rais kwa watanzania waishio nje ya nchi, Mtaalamu wa Uchumi Dr. Bravious Kahyoza anasema Diaspora ni muhimu kwenye uchumi wa Taifa lolote huku akiona hatua hiyo kuongeza mchango wao katika uchumi wa nchi.
“Diaspora ni muhimu sana kwenye uchumi wa nchi yoyote. Hii ni hatua nzuri na itaongeza mchango wao kwenye uchumi wa nchi. Italeta ujuzi ambao wanao na kuweza kufingua fursa zaidi. Kwa sasa pesa inayotumwa na Diaspora kwenye uchumi wetu ni ndogo, wastani wa usd 800 million kwa mwaka sawa na 0.9% ya GDP Hiki ni kiwango cha chini kuliko nchi jirani za Uganda na Kenya.”
Pia Rais ametoa maelekezo kwa wizara ya nje kutoa mafunzo ya sera hii kwa taasisi za Umma ndani ya nchi ili watumishi wajue jinsi sera hiyo inavyogusa majukumu yao ya kila siku. Katika maagizo hayo Rais alitaka timu ya mabalozi wastaafu watumike katika kazi ya kutoa elimu.
“Baada ya kuandaa mkakati wa sera hii, na kukamilisha uandaji wa mwongozo wa diplomasia ya uchumi utakaotafsiri sera hii, hatua itakayofuata sasa niwatake muendelee na utoaji wa mafunzo ya elimu ya sera hii kwa taasisi za Umma kuhusu maudhui ya sera.” Alisema Mheshimiwa Rais akitoa maagizo mahsusi baada ya uzinduzi wa sera.
Kuhusiana na suala la utoaji wa elimu ili sera hii iweze kueleweka, Mtaalamu wa Uchumi na mchambuzi wa masuala ya kiuchumi na kisiasa Dr. Kahyoza anasema ni muhimu kwa taasi za serikali kuwa na uelewa wa sera yetu ili kulinda uchumi na usalama wa taifa.
“Kuelewa mambo haya kwa taasisi za serikali ni jambo mahsusi kwa uchumi, usalama na maendeleo ya nchi. Maagizo haya yataleta mapinduzi ya fikra juu ya wataalam wa serikali wanavyoitazama dunia katika kulinda maslahi ya nchi yetu.” Alisema Dr. Kahyoza.
Katika hatua nyingine, Rais Samia ametoa maelekezo kwa wizara mbalimbali kuangalia sheria ili ziwezeshe vijana kwenda kujiajiri nje ya nchi zinapotokea fursa mbalimbali. Tulitaka kufahamu kutoka kwa mtaalamu wa Uchumi, je, hii ina maanda gani wakati kukiwa na changamoto ya ajira hapa nchini Tanzania?
“Labour export ni suala la wazi na lazima kwa uchumi wa kileo. Kwenye dunia iliyofungamana sana(Glocal) wanasema unafikiria ukitazama ndani lkn ukitenda kama dunia. Hili ni eneo la vijana” Alifafanua Dr. Kahyoza.
Sera ya mambo ya nje nchini Tanzania inaratibiwa na kusimamiwa kwa kiasi kikubwa na wizara ya mambo ya nje. Kwa sasa Watanzania wanasubiri utekelezaji wa sera hii baada ya kukamilika kwa mikakati na miongozo yake.
About The Author
Last modified: May 21, 2025