Visit Sponsor

Written by 4:44 pm KITAIFA Views: 7

MFUKO WA TAIFA WA MAJI WAFANIKISHA MIRADI 354 MIJINI NA VIJIJINI

Afisa mtendaji mkuu wa mfuko huo, Wakili Haji Mandule akizungumza na wahariri pamoja na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari, Dar es Salaam Oktoba 31, 2024

Mfuko wa Taifa wa Maji nchini (National Water Fund) ambao uko chini ya Wizara ya Maji umefanikisha kukamilika kwa miradi  karibu 354 kuanzia Julai 2021-Juni 2024 ikiwemo ya usambazaji maji na usafi wa mazingira mijini na vijijini.

Akizungumza na waahariri pamoja na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Salaam Oktoba 31, 2024, Afisa mtendaji mkuu wa mfuko huo, Wakili Haji Mandule amesema  kuna mafanikio mengi yamepatikana tangu taasisi hiyo ianze hasa katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya 6 chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Vilevile tumefungua dirisha la mikopo ya gaharama nafuu, riba yetu ikiwa ni asilimia 6, Serikali huwa mara nyingi inawekeza kwenye miundombinu mikubwa, na kama mnavyofahamu siyo mamlaka zote zinakidhi vigezo vya kukopa kwenye mabenki, Mfuko wa Maji unakuja kuleta suluhu katika hilo eneo, tunatoa mikopo, mpaka Julai 2024 tulikuwa tumetoa bilioni 5.3, vilevile tuna maombi ya karibu bilioni 13 yapo kwenye hatua mbalimbali yanafanyiwa uchakataji,” amesema Mandule..

Aidha mtendaji huyo amesema sheria inaelekeza asilimia 85 ya fedha wanazopokea Mfuko wa Taifa wa Maji ziende kwenye miradi na tangu taasisi yao ianze asilimia karibu 90 yote wanaipeleka kwenye utelekezaji wa miradi ya usambazaji maji na usafi wa mazingira mijini na vijijini kwa maana ya ile ya RUWASA pamoja na ya mamlaka ya maji na utunzaji wa vyanzo vya maji ambapo watu karibu milioni 5.3 wanafaidika na utekelezaji wa miradi hiyo.

“Kama mnavyofahamu mamlaka za maji zinakuwa na mahitaji makubwa ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika maeno yao, baadhi ya miradi ambayo tumeitekeleza katika kipindi hiki, ni pamoja na ule mkubwa wa Isaka Kagongwa ambao uko Shinyanga, wanufaika wake ni karibu watu 62,206, Katoro Buseresere uliyopo Geita ambao umetumia karibu bilioni 2.5 watu karibu153,000 wananufaika, pia Kemondo Bukoba kwa kifupi karibu kila mkoa ndani ya Tanzania utakuta kuna miradi ambayo imepokea fedha kutoka Mfuko wa Taifa wa Maji”, amesema.   

Pia Wakili Mandule amesema mbali na kupata fedha kutoka sehemu mbalimbali chanzo kikubwa cha mfuko wao ni tozo ya kwenye kila lita ya mafuta ya dizeli na petrol shilingi 50 na kwamba wameingia makubaliono na benki ya TIB, ambayo ndiyo inasimamia mfuko huo kwa niaba yao, taasisi inayotaka kukopa inapitia katika benki hiyo huku mikopo wakilenga zaidi kwenye mamlaka za maji, kwa mujibu wa sheria zinatakiwa zijiendeshe kibiashara, hazitakiwa kutegemea ruzuku kutoka Serikalini kwasababu zinatoa huduma na wananchi wanalipia.

About The Author

(Visited 7 times, 1 visits today)

Last modified: October 31, 2024

Close