Visit Sponsor

Written by 12:47 pm KITAIFA Views: 8

OSHA WAFUNGUKA MAFANIKIO MIAKA MITATU YA RAIS SAMIA

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam

WAKALA wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), umesema kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu wamepata mafanikio makubwa ikiwemo kuongeza maoneo ya kazi yaliyosajiliwa hadi kufikia 30,309.

Akizungumza na wahariri pamoja na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda amesema kuwa miaka mitatu wameweza kuimarisha shughuli za usimamizi wa usalama na afya mahali pa kazi nchini. Mafanikio hayo yameainishwa ikiwa ni mwendelezo wa taasisi zilizopo chini.

“Katika kipindi tajwa, wakala umefanikiwa kuongeza idadi ya maeneo ya kazi yaliyosajiliwa kutoka 4,336 hadi 30,309, ongezeko hili ni sawa na asimilia 599.

Aidha idadi ya kaguzi zilizofanyika zimeongezeka kutoka kaguzi 104,203 hadi kufikia kaguzi 776,968 sawa na asilimia 646,”alisema.

Amesema kaguzi hizo zinahusisha, ukaguzi wa jumla, ukaguzi maalum kama vile ukaguzi wa usalama wa umeme, Vyombo vya Kanieneo, ukaguzi wa vifaa vya kunyanyulia vitu vizito, ukaguzi wa kiegonomia pamoja na tathmini ya vihatarishi vya kimazingira.

Mwenda pia ameongezea kuwa kumekuwa na ongezeko la asilimia 44.1 ya wafanyakazi waliopata mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kutoka wafanyakazi 32,670 hadi kufikia 47,090.

“Mafunzo haya yanajumuisha mafunzo ya usimamizi wa masuala ya usalama na afya mahali pa kazi na uundwaji wa Kamati za Usalama na Afya, mafunzo ya kufanya kazi katika maeneo ya juu, Mafunzo ya Huduma ya Kwanza, Mafunzo ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali katika maeneo ya kazi, Mafunzo ya Usalama na Afya katika sekta za Mafuta na Gesi pamoja na sekta ya Ujenzi na Majenzi na Mafunzo ya Uendeshaji Salama wa Mitambo,” amesema.

Mwenda amesema pia OSHA imeboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini yametokana na uongozi wake madhubuti wa Rais Samia yanayoendana na utekelezaji wa Ilani ya Chama Tawala Ibara ya 130 (f) ambapo chama kimewaahidi Watanzania kwamba kitajenga uwezo wa waajiri na wafanyakazi kuhusu afya na usalama mahali pa kazi.

“Wote ni mashahidi na tunaona juhudi ambazo, Rais wetu, amekuwa akizifanya kuhakikisha kuwa wawekezaji wanakuja kuwekeza nchini ikiwemo kuhimiza uboreshaji wa mazingira ya biashara na uwekezaji na hili ni pamoja na maelekezo mbalimbali katika hotuba zake na hata hivi karibuni tumeona katika mabadiliko aliyoyafanya kwenye miundo ya wizara, suala la uwekezaji limepewa kipaumbele na kuhamishiwa katika Ofisi ya Rais,” amesema.

Amesema OSHA itahakikisha uwekezaji nchini unakuwa na tija na manufaa kwa wananchi pamoja na kulinda nguvukazi ya Taifa, ili kuwa na uzalishaji endelevu.

About The Author

(Visited 8 times, 1 visits today)

Last modified: December 8, 2023

Close