Bondia Hassan Mwakinyo ambaye amefungiwa mwaka mmoja na faini milioni moja
Bondia wa ngumi za kulipwa nchini mwenye maskani yake jijini Tanga, Hassan Mwakinyo amefungiwa kujihusisha na mchezo huo kwa kipindi cha mwaka mmoja huku akitakiwa kulipa faini ya shilingi milioni moja na chama cha mchezo huo, Tanzania Professional Boxing Regulatory Commission (TPBRC) kwa kosa la kukiuka mkataba wa kazi.
Akisoma hukumu hiyo mbele ya Waandishi wa Habari, jijini Dar es Salaam Oktoba 10, 2023, Katibu Mkuu wa Kamisheni ya ngumi za kulipwa, George Silas Lukindo alisema kuwa Mwakinyo amekutwa na hatia kwa kitendo cha kugomea kupanda ulingoni bila sababu zenye mashiko na kwamba amekiuka mkataba wake na kampuni ya Puff Sport Promotion (waandaaji), kupitia kifungu cha 14 cha mkataba huo ambacho kinaeleza ni kipi kinapaswa kufanyika iwapo bondia anakiuka mkataba wake na mkuzaji.

Katibu Mkuu wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa nchini, George Silas Lukindo
“Kwa mujibu wa kanuni za adhamu za Kamisheni ya kusimamia ngumi za kulipwa (TPBRC), hasa kifungu cha nne, kifungu kidogo cha nne, tano kinachoeleza kuwa kushindwa kuheshimu mkataba kunapelekea muhusika kupewa adhabu ya kulipa faini isiyopungua shilingi za Kitanzania laki 3 na isiyozidi shilingi za Kitanzania milioni 1, pamoja na gharama za mkataba.
Pili kufungiwa kwa muda wa miezi sita au mwaka mmoja au adhabu zote kwa wakati mmoja. Kwa kukataa kwake kupanda ulingoni ni dhahiri amekiuka kifungu hicho na adhabu yake ni kufungiwa mwaka mmoja kutoka leo tahere 5, 10, 2023 hadi tarehe 5, 10, 2024 na kulipa faini ya milioni moja kupitia akaunti ya kamisheni haraka iwezekanavyo” alisema Silas.
Pia aliweka wazi kuwa msingi mkuu wa kutoa adhabu hiyo ni kwamba, bondia Hassan Mwakinyo ni mkubwa hapa nchini ambaye angepaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha anakuwa mfano bora kwa mabondia wengine wanaochipukia, kitendo chake cha kujichukulia maamuzi bila kuheshimu mkataba hakina afya kwa maslahi mapana ya maendeleo ya mchezo wa ngumi za kulipwa nchini.
“Pia Mwakinyo anapaswa kujifunza namna ya kuheshimu uongozi na viongozi wake kwa kupewa onyo kali baada ya kuonesha tabia isiyoridhisha wakati kiongozi mkuu wa kamisheni akiongea naye. Hassan Mwakinyo alipelekea kutoa maneno machafu yasiyo na stara mbele ya wajumbe wa kikao hicho. Hii siyo kwa Mwakinyo, kwa mabondia wote nchi nzima, hakuna ambaye yuko juu ya kamisheni, tunawaomba wote waheshimu utaratibu ambao upo kwenye mkataba, hatutasita kumchulia hatua mtu yeyote mwenye lengo la kuichafua Kamisheni ya ngumi Tanzania” alisema Katibu Silas.
About The Author
Last modified: October 10, 2023